Mapema, kabla ndege haijaondoka na baada ya kuagana na maafisa waliomsindikiza, Nanda aliingia katika ndege na kutafuta namba ya kiti chake. Alivyoiona, alishtuka. Msichana mrembo alikaa kando ya kiti (cha Nanda) akiongea na simu, mara ya mwisho kabla ya kuondoka. Alivyofika, Nanda hakujizuia kuchangamka – alitupa tabasamu. Alivyoliona, kupitia miwani myeusi, binti alitabasamu pia, meno yake yakimchanganya kamishna. Alimsalimia Nanda, harakaharaka, na kurudi katika simu huku Nanda akikaa (vizuri) na kumsubiri. Alivyokata simu, alitoa miwani na kumwomba radhi Kamishna Nanda. Nanda akamwambia asijali, huku akitabasamu. Alikuwa na safari ya Bama kupitia Tailandi, kwa ndege ya Shirika la Ndege la Skandinavia na Maxair kutokea Bangkok; sawa kabisa na safari ya kamishna.