Kolonia Santita imesambaa dunia nzima. Hapa Meksiko wana magenge rafiki zaidi ya mia moja yakiwemo makubwa kabisa katika Latino ya Matamolos na Baja California. Nikitekwa nyara na memba yoyote wa magenge hayo, kuna uwezekano mkubwa wasinifanye chochote au nisilipe chochote kwa sababu ya Wanda. Fadhila ya uhalifu. Kwa sababu ya fadhila ya uhalifu; baba, au viongozi wengine wa serikali ambao watoto wao wamo ndani ya 'mpango' huo, wanatakiwa wawakingie kifua (kwa namna yoyote wanayoweza) pindi wanapoanguka katika mikono ya dola na sheria. Wasipofanya hivyo kutakuwa na vita ya ndani kwa ndani … kama unanielewa. Hivyo, kuna mtu anaitwa El Tigre – baba yake Wanda – ndiye ninayetaka unisaidie. Amemuua Marciano, na watu wengi wa Meksiko. Nataka kumlipia kisasi Marciano, na marafiki zangu wengi ambao El Tigre amewaua, hata kwa njia isiyodhahiri.